Thursday, September 02, 2004

Karibuni Nyumbani Madereva Watatu

Karibu nyumbani Jalal Ahmed!
Vipi mambo Faiz Salim?
Habari gani Ibrahim Iddi?

Karibuni nyumbani Wakenya wenzetu
Poleni sana kwa vituko vya kushtua
Wahenga walivyonena
Subira huvuta heri
Kisha wakaongeza
Baada ya dhiki faraja
Kote ulimwenguni ni tafrija
Popote Wakenya wapatikanapo
Twaona nyuso zilozojaa furaha
Badala ya majonzi ni kutabasamu

Wacha tupumue leo,
wacha tuwangue kicheko
Wacha tuwike na vigelegele
Nadhani leo huko
Sarigoi na Mwembe Kuku
Majengo Sidiria na Ngomeni
Kongowea na Changamwe
Kote jijini Mombasa
Wanawake na Wanaume
Vijana kwa Wazee
Wanaruka ruka huku wakicheza
Kirumbizi na Chakacha

Tumepokea habari moto moto
Kutoka mbali kule ghuba Arabuni
Wenzetu wameachiliwa
Baada ya kuzuiliwa
Zaidi ya mwezi na masiku kadhaa
Ndani ndani huko Irak

Hebu mtizame Dada Samira

Leo anacheka na kusherekea
Badala ya kulia na wasiwasi

Mwangalie Bi Hidaya

Leo anatabasamu na shukrani
Badala ya kupapatika na hofu

Mshangilie Aisha

Leo ana furaha karibu kuzimia
Badala ya kuhangaika bila usingizi

Wakenya nchini
na wale waliorundika ughaibuni
Wanashukuru wote wale
Mabalozi, waandishi, mashehe na maimamu
Wanakereketa duniani waliofanya hala hala
Wakiwasihi watekaji nyara wasiwakate vichwa
Wenzetu watatu madereva walioajiriwa huko Kuwait
Mimi mwenyewe najuimika na wananchi wenzangu
Nikiwakaribisha na kuwapigia pole
Wakenya na wenyeji wa Mombasa wenzangu
Sina mengi leo hapa jijini Montreali
Ijapokuwa kutuma ujumbe kuwakaribisha
Madereva wetu watatu nyumbani

Onyango Oloo
Mkoani Quebec
Jumatano,
Septemba Mosi, Mwaka wa Elfu Mbili na Nne

No comments: